
Watu zaidi ya 21 wamekufa katika Kata ya Pinyinyi wilayani Ngorongoro mkoani Arusha kwa ugonjwa wa ajabu wa kutapika damu.
Mtendaji wa kata hiyo, James Mushi
alibainisha kuwapo kwa ugonjwa huo wakati akisoma risala kwa Mkuu wa
Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alipokwenda kutembelea kata hiyo kujionea
shughuli za maendeleo, ikiwa ni ziara ya siku tano katika wilaya hiyo.
Baada ya Mushi kueleza katika risala
yake juu ya kuwepo kwa ugonjwa huo kwa zaidi ya miaka minne na watu 21
kupoteza maisha, ndipo mkuu wa mkoa alipomsimamisha Mganga Mkuu wa Mkoa
ili kupata maelezo ya kwa nini mkoa haujachukuwa hatua.
Mganga huyo alisimama na kuueleza umma
wa wananchi waliohudhuria mkutano huo wa hadhara kuwa hana taarifa ya
kuwepo kwa ugonjwa huo na wala mkoa hauna taarifa juu ya kuwepo kwa
ugonjwa huo.
Majibu hayo yalimchanganya na
kumkasirisha mkuu wa mkoa na kuamua kumsimamisha Mganga wa Wilaya ya
Ngorongoro (DMO), Omari Sukari kutoa majibu kama na yeye hana taarifa ya
kuwepo kwa ugonjwa huo.
Sukari alikiri kuwepo kwa ugonjwa huo na
kweli umeua watu 21 na amefanya jitihada na ziada kwa kupeleka sampuli
Wizara ya Afya kwa wataalamu, kwani hata yeye ameshindwa kujua nini
chanzo cha ugonjwa huo na kinasababishwa na kitu gani.
Mganga huyo wa wilaya alisema vipimo vya
awali vilionesha kuwa ugonjwa huo husababishwa na ugonjwa wa kichocho,
lakini bado wamejiuliza zaidi kwa kupeleka sampuli nyingine ya matapishi
kwa wataalamu wa magonjwa ya binadamu kujua zaidi ukweli wa ugonjwa huo
na majibu hayajarudi.
Baada ya majibu hayo, mkuu wa mkoa
alieleza waziwazi kusikitishwa na kushangazwa majibu ya Mganga Mkuu wa
Mkoa wa Arusha na kusema kuwa haingii akilini ugonjwa ulioua watu 21 na
uko zaidi ya miaka minne katika Kata ya Pinyinyi, lakini hana taarifa
wakati mganga wa wilaya anayo taarifa.
Gambo alisema hiyo inaonesha wazi kuwa
baadhi ya watumishi wa serikali mkoani, wanafanya kazi kwa mazoea na
kushindwa kujua ama kupata taarifa za kila siku katika wilaya.
Alisema hilo hatalivumilia hata kidogo
na kuwataka wakuu wa idara wa mikoani, kuwajibika kwa kupata taarifa za
kila siku katika wilaya zote za Mkoa wa Arusha ili majibu ya kila kitu
yapatikane na kupatiwa ufumbuzi wa kutosha.
“Hii ni aibu, ugonjwa upo kwa miaka
minne na tayari umeua watu 21, lakini RMO hana taarifa, lakini DMO anayo
taarifa na amefanya kazi ya ziada kutafuta chanzo cha ugonjwa huu,”
alisema mkuu wa mkoa.
“Kama nisingekuja hapa ina maana huu
ugonjwa usingejulikana wala kupata majibu ya kutosha na watu
wangeendelea kufa, sasa nataka RMO kuhakikisha ugonjwa huo unakwisha na
dawa inapatikana,” alisema Gambo.
Katika risala hiyo, wananchi
wamempongeza mkuu huyo wa mkoa kwa kufika katika kata hiyo, kwani mara
ya mwisho Mkuu wa Mkoa wa Arusha kutembelea kata hiyo alikuwa Mohamed
Babu mwaka 2006.
