Hukumu hiyo ya kesi ya madai namba 14 ya mwaka 2015 dhidi ya Mukesh, ilitolewa Alhamisi ya wiki iliyopita na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Wilbert Chuma baada ya kumwona mfanyabiashara huyo kuwa na hatia kwa kushindwa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.
Hakimu Chuma alisema kulingana na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka, mahakama imeridhika bila kuacha shaka kuwa Mukesh ana hatia na hivyo atatakiwa kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya shilingi elfu 50,000.
“Kulingana na ushahidi uliotolewa mahakamani na upande wa mashitaka, mahakama imemwona mdaiwa kuwa na hatia baada ya kushindwa kulipa kodi halali kwa mujibu wa kanuni ya 17 (1) (a) ya Sheria za Halmashauri ya Jiji la Mwanza ya mwaka 2008 ya gharama za tozo,” alisema Chuma.
Awali akijitetea kwa nini asipewe adhabu kali, Mukesh alisema yeye ni mzee mwenye umri mkubwa na anategemewa na familia hivyo mahakama isimpe adhabu kali kutokana na sababu hizo.
Kabla ya hukumu hiyo, mwendesha mashitaka wa serikali, Lameck Merumba aliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo ya kukiuka na kuvunja sheria. Hadi gazeti hili linatoka mahakamani hapo, mfanyabiashara huyo alikuwa akifanya taratibu za kulipa faini hiyo.
