
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ameomba Jumuiya ya Kimataifa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupiga vita ujangili.
Profesa Maghembe amesema hayo leo, eneo la Matambwe Selous kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya ndege maalumu nane zisizo na rubani zilizotolewa na Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF).
Ndege hizo zitatumika katika Pori la Akiba la Selous kuimarisha ulinzi wa wanyamapori kwa kukusanya taarifa za kiintelijensia, zitakazosaidia kukamatwa majangili. Ndege hizo zina thamani ya dola 80,000 za Marekani (Sh172 milioni).
“Msaada huu umekuja wakati mwafaka, Pori la Akiba la Selous linahitaji teknolojia za kisasa kuimarisha mapambano dhidi ya ujangili ndani na kuzunguka hifadhi hii,” amesema Proesa Maghembe.
