» » Lindi watengewa bil. 5.6/- kuboresha mawasiliano

ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO


SERIKALI kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote, imetenga dola za Marekani 2,186,061 (Sh bilioni 5.6) ili kupeleka mawasiliano katika kaya 25 mkoani Lindi zilizokuwa na huduma duni na zile zilizokosa kabisa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani alisema hayo bungeni mjini hapa jana, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Hamida Mohammed Abdallah (CCM) aliyetaka kujua ni lini Serikali itaboresha ujenzi wa minara ya huduma za mawasiliano ya simu katika vijiji vya mkoa huo wa Lindi.

Katika swali lake la msingi, Hamida alisema, kwenye karne hii ya sayansi na teknolojia, mawasiliano ya simu za mkononi ni muhimu katika kurahisisha huduma mbalimbali kwa watumiaji wakiwemo wavuvi, wafanyabiashara, wafanyakazi, wasanii na wengine.

Kutokana na hilo, aliuliza ni lini Serikali itaboresha ujenzi wa minara ya huduma ya mawasiliano ya simu katika vijiji vya mkoa huo.

Akijibu, Ngonyani alisema mawasiliano ya simu za mkononi ni muhimu katika kurahisisha na kurahisisha maendeleo, hivyo Serikali imeweka sera madhubuti kuhakikisha wananchi katika maeneo yote ya nchi wanapata huduma hiyo.

Kwa mujibu wa Ngonyani, kwa kutambua hilo, Serikali imeanzisha mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF), ili kutekeleza sera hiyo kwa kupeleka huduma za mawasiliano kwenye maeneo yote yenye uhitaji wa huduma hiyo.

“Serikali kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote imetenga Dola za Marekani 2,186,061 kwa ajili ya kupeleka mawasiliano kwenye kaya 25 za Lindi zilizokuwa na huduma duni pamoja na zilizokosa kabisa huduma za simu za mkononi,” alisema Naibu Waziri.

Aliongeza kuwa, kati ya kata hizo, kata ya Kiegei wilayani Nachingwea imekwishapata mawasilianoi ya simu za mkononi kupitia kampuni ya TTCL wakati kata zingine ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano.

Alisema, Serikali kupitia mfuko huo wa mawasiliano itaendelea kuyaainisha maeneo mengine ya mkoa wa Lindi na Tanzania kwa ujumla, kadri ya uhitaji na upatikanaji wa fedha katika kufanikisha malengo ya uanzishwaji wa mfuko, ambayo ni pamoja na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za mawasiliano ili kurahisisha na kuharakisha huduma za maendeleo.
ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO

About Mashak

About Mzalendo Huru Staff:

Send us your articles, questions, feedback, suggestions, press releases and all others to Whats app on +255657905751
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post