Na Imelda Mtema, UWAZI
Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Amina Ahmad (45) mkazi wa Magomeni Chama jijini Dar, yuko katika mateso makali sana kwa muda wa miaka 21 baada ya uvimbe uliokuwepo tumboni kumsumbua huku akiwa hajaweza kwenda hospitali hata siku moja.
Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Amina Ahmad (45) mkazi wa Magomeni Chama jijini Dar, yuko katika mateso makali sana kwa muda wa miaka 21 baada ya uvimbe uliokuwepo tumboni kumsumbua huku akiwa hajaweza kwenda hospitali hata siku moja.
Akizungumza na gazeti hili kwa uchungu
mama huyo amesema tatizo hilo lilimuanza tangu 1995, ambapo kilianza
kitu kama kipele kidogo lakini siku zilivyozidi kusonga kikawa
kinaongezeka lakini alikuwa akiona ni hali ya kawaida.
“Mara ya kwanza niliona ni jambo la
kawaida sana lakini siku zilivyosonga ndivyo nilivyoona kinazidi kukua
kitu ambacho kilianza kunipa shaka kidogo,” alisema Amina.
Mgonjwa huyo aliendelea kuzungumza kuwa
maisha yake ni duni sana hana kipato chochote cha kumuwezesha kwenda
kutibiwa hospitali kwa kuwa anajua ataambiwa inapaswa kufanyiwa upasuaji
wakati hana uwezo wa fedha kwani hela anayopata kwa siku ni ndogo sana
tena ya mlo mmoja.
“Yaani natamani sana hospitali hata
wajue hili tatizo lakini sina hela hata ya kuanzia kwa sababu kipato
changu ni cha chini sana tena cha mlo mmoja tu na wakati mwingine
usiwepo,” alisema.
Aliendelea kusema kuwa amekuwa mtu wa
kulala kwa kuwa hawezi kufanya kazi nzito kwa sababu ya maumivu makali
anayopata na kuna wakati anatapika mpaka kupoteza nguvu na kuanguka
chini ambapo husaidiwa na mwanaye wa miaka tisa.
“Kwa jinsi uvimbe huu unavyonitesa
nahisi siku moja utapasuka na kusababisha nikapoteza maisha na kumuacha
mwanangu akiteseka kama mimi mama yake,” alisema Amina kwa huzuni.
Msomaji wetu, Amina yupo katika mateso
makali hivyo anaomba msaada wako ili aweze kwenda hospitali kupata
matibabu kisha aendelee na shuguli zake za kila siku akiwa mwenye afya
njema na furaha kama wewe.
Kama umeguswa na tatizo lake unaweza
kumtumia mchango wako kupitia namba zake ambazo ni 0716 416144 au
0783414944 na Mungu atakubariki.
