» »Unlabelled » Simba kumchunguza Okwi kabla ya kumsajili

ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO

Akizungumza na Nipashe jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe, alisema kuwa kwa kuwa mshambuliaji huyo aliondoka kwenye klabu yake ya Sonderjyske ya Denmark akiwa hajacheza michezo mingi, kama watataka kumsajili watalazimika kuchunguza kiwango chake kwanza.

Okwi aliyezaliwa Desemba 25,1992 alivunja mkataba wake na klabu hiyo ya Denmark aliyokuwa amejiunga nayo Julai, 2015, baada ya kuona hapati nafasi ya kucheza.

Mkataba wa Okwi klabuni hapo ulikuwa umalizike katikati ya mwaka 2020 baada ya kusaini mkataba wa miaka mitano.

“Okwi ni mchezaji wetu na Simba ni nyumbani kwake. Milango ipo wazi kwake kurejea, lakini litakapofika suala la kusajiliwa tena, lazima Kamati ya Ufundi ijiridhishe kuhusu kiwango chake,”alisema Hans Poppe.

Hata hivyo, kama Simba itamsajili mshambuliaji huyo itawalazimu kusubiri mpaka msimu ujao wa ligi kuu kuweza kumtumia kwa kuwa kanuni za ligi kuu haziruhusu mchezaji anayesajili nje ya vipindi viwili vya usajili katika msimu kutumika kwenye msimu husika.

Dirisha dogo la usajili kwa Tanzania lilifungwa Desemba 30 na kwa sasa hakuna mchezaji anayeweza kusajiliwa akatumika.

Okwi aliyeifungia timu yake ya taifa mabao 18 katika michezo 35 aliyoichezea, aliondoka Simba baada ya nusu msimu tu tangu arejee akitokea kwa mahasimu wao, Yanga ambako pia alicheza kwa nusu mwaka kabla ya kutofautiana na viongozi wa klabu hiyo na kuondoka.

Simba ndiyo iliyomuingiza Okwi Tanzania mwaka 2010 akitokea SC Villa ya kwao Uganda, alicheza Msimbazi hadi mwaka 2013 aliponunuliwa na Etoile du Sahel ya Tunisia kwa dola za Kimarekani 300,000 (zaidi ya shilingi milioni 600 kwa wakati huo).

Hata hivyo, Okwi aliondoka Tunisia baada ya miezi mitatu kufuatia kutofautiana na uongozi wa klabu hiyo na baadaye kufungua kesi FIFA akiomba aruhusiwe kucheza klabu nyingine kulinda kipaji chake wakati mgogoro wake na Etoile unaendelea.

Etoile ilisitisha huduma kwa Okwi, baada ya kukerwa na desturi ya mchezaji huyo kuchelewa kurejea kujiunga na timu anaporuhusiwa kwenda kujiunga na timu yake ya taifa Uganda.

Akasaini tena SC Villa katikati ya mwaka 2013 kabla ya Desemba mwaka huo, kuhamia Yanga huku kesi yake na Etoile ikiendelea FIFA.
ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO

About Mashak

About Mzalendo Huru Staff:

Send us your articles, questions, feedback, suggestions, press releases and all others to Whats app on +255657905751
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post