Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima katika ufafanuzi alioutoa jana, alisema kuwa wapiga kura walioandikishwa katika jimbo la hilo ni 9,275 kati ya hao wapiga kura 6,406 walijitokeza kupiga Kura siku hiyo ambapo kura halali zilikuwa 6,172. Aidha, alisema kati ya kura hizo, kura zilizoharibika zilikuwa 234.
Mbali na uchaguzi wa ubunge Dimani, kata 22 Tanzania Bara nazo zilifanya uchaguzi wa madiwani. Katika uchaguzi huo mgombea wa CCM, Juma Ali Juma aliibuka mshindi kwa kura 4,860 huku mpinzani wake wa CUF, Abdulrazak Khatib Ramadhan akipata kura 1,234.
Mkurugenzi huyo alisema katika uchaguzi huo vyama 11 vilikuwa na wagombea wa ubunge ambapo chama cha ACT-Wazalendo kilipata Kura 8, ADC kura 42, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kura 4,860, CHAUMA kura 10, Chama Cha Wananchi (CUF) kura 1,234 na chama cha DP kura 8.
Vyama vingine ni NRA kura 1, SAU kura 4, TLP kura 2, cha UMD Kura 2 na UPDP kura 1 na kufanya jumla ya kura za vyama vyote kuwa 6,172.
Uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Dimani, Zanzibar unafanyika kutokana na kifo cha Mbunge wa jimbo hilo, Hafidh Ali Tahir aliyefariki alfajiri ya kuamkia Novemba 11, mwaka jana kwenye Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.