Kutokana na tukio hilo, Polisi inawashikilia askari sita wa Suma JKT kwa uchunguzi dhidi ya tukio hilo lililotokea Kijiji cha Kandaskirieti Kata ya Oldonyosambu Tarafa ya Mukulati huku miili ya watu wanne waliokufa kutokana na shambulio hilo, ikiwa imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo akizungumzia tukio hilo, alisema juzi saa 11 jioni katika Kijiji cha Kandaskirieti, watu wanne walikufa baada ya kupigwa risasi na askari wa Suma JKT.
Alisema taarifa za awali zimebaini kuwa askari hao wa Suma JKT ambao ni walinzi wa shamba la miti la serikali la Meru Usa Plant, walianza kufanya operesheni ya kuondoa mifugo, ambako walikamata ng’ombe 45, mbuzi na kondoo 65 kisha kuwapeleka zizi la serikali lililopo Kituo cha Polisi Oldonyosambu.
Alisema saa 11 jioni waliendelea tena na operesheni hiyo na kukamata ng’ombe wengine 80, mbuzi na kondoo wakiwa 70 na kuwapeleka kwenye zizi la serikali na wakati wanarudi, ndipo walipokutana na kundi la wananchi wakiwa na silaha mbalimbali za jadi na kuanza kushambuliwa, hivyo askari hao walirusha risasi hewani ili kuwatawanya.
Aliongeza kuwa lakini askari hao walipokuwa wakiwatawanya wananchi hao, waliendelea kuwashambulia, ndipo na wao walipoamua kuwapiga risasi na watu wanne walifariki dunia huku wengine watano wakijeruhiwa.
Kamanda Mkumbo aliwataja waliokufa kuwa ni Mbayani Melau (27), Julius Kilusu (45), Lalashe Meibuko (25) na Seuri Melita (32) ambao miili yao imehifadhiwa Mount Meru.
Pia aliwataja majeruhi waliojeruhiwa kwenye tukio hilo kuwa ni William Ngirangwa (29), Mathayo Masharubu (34), Julius Lazaro (32), Evelyn Melio (28) na Isaya Thomas (13), ambao wamelazwa Mount Meru wakiwa wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao huku hali zao zikiwa si nzuri.
Akisimulia tukio hilo, mwanafunzi huyo Thomas alisema alitoka shule vizuri juzi na kwenda kwao na alifika vizuri nyumbani, kisha baada ya muda akiwa Oldonyosambu madukani, alishangaa kuona askari wakifyatua risasi ovyo karibu na watu waliokuwa wakishangaa tukio hilo.
“Mimi nimetoka shule sijui lolote wakati nashangaa tukio hili nami nimejikuta nimepigwa risasi mgongoni na mpaka sasa sijapata matibabu nasubiri kupewa huduma, lakini sijui lolote kuhusu tukio hili kilichoniponza ni kushangaa ni kwa nini watu wanapigwa risasi,” alibainisha mwanafunzi huyo.
Majeruhi mwingine, Julius Lazaro (32), alisema alikuwa kijiweni eneo la Oldonyosambu madukani ghafla walishangaa kuona askari wakishuka na kuuliza nani amewapiga mawe, na kuwajibu kuwa hawajui ndipo walipoambiwa watawanyike na walipotawanyika ghafla alishangaa kusikia milio ya risasi na yeye kujeruhi wa mguuni.
“Hawa askari walikuwa ni mchanganyiko maana waliwapiga watu risasi bila kujali wanahusika na tukio hili au la. Ukweli tumepigwa risasi tusiostahili kama ni operesheni ya kukamata mifugo msituni kwa nini siye wengine tupigwe risasi ovyo na hapa hospitali wanahitaji hela na sisi hatuna sasa sijui hizi risasi tulizonazo itakuwaje,” alieleza Lazaro.
Akizungumzia tukio hilo, Diwani wa Kata ya Oldonyosambu, Raymond Lairumbe alisema ni la juzi kati ya saa 11 na 12 jioni, ambako kulikuwa na oparesheni ya kuondoa mifugo kwenye shamba la Meru Usa Plant ambalo ni shamba la miti la serikali.
“Hawa askari walikamata ng’ombe na mbuzi asubuhi kisha kuwaswaga na kuwapeleka Kituo cha Polisi Oldonyosambu, lakini jioni walikwenda msituni tena na kuanza kuwapiga hao watu waliokufa kisha kuanza kupiga risasi ovyo wananchi wangu ambao wengine wamekufa wengine ndio majeruhi akiwemo mwanafunzi,” alidai diwani.
Alisema wananchi hao hawatazika miili hiyo hadi hapo viongozi wa serikali, watakapofika na kuzungumzia suala hilo, kwani wengine wamepigwa risasi bila ya makosa na walikuwa wakitoka kwenye shughuli zao.