» »Unlabelled » RC Mbeya asisitiza zuio ugawaji viwanja U/Ndege

ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO

 Wednesday, December 28, 2016

SERIKALI mkoani Mbeya imesisitiza kuwa msimamo wa kuzuia ugawaji na urasimishaji wa viwanja vya makazi katika eneo la akiba la uwanja wa ndege wa zamani wa Mbeya uko pale pale na itaendelea kuusimamia mpaka pale mwafaka mbadala utakapofikiwa.

Sambamba na hilo, pia imesema inaendelea na utaratibu wa kuchunguza dalili za rushwa inayotajwa kuwepo wakati wa upimaji wa viwanja, ikidaiwa wataalamu walioshiriki waliahidiwa kupewa ofa ya viwanja 10 endapo wangeharakisha mchakato huo na kuwapa hati watu wanaodai kuwa wamiliki wa eneo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Iyela jijini hapa baada ya kukagua uwanja wa ndege wa zamani wa Mbeya akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.

Alisema msimamo wa serikali ya mkoa ni kuona eneo la akiba na uwanja wa ndege wa zamani linalindwa kwa kuwa mamlaka ya viwanja vya ndege bado inayahitaji maeneo hayo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za anga.

Alisema kwa kuwa serikali inaendelea kufuatilia sakata zima la ugawaji wa viwanja vya makazi kwenye eneo hilo, wahusika wa mgogoro huo hawana budi kuvuta subira kwakuwa baada ya vyombo vya sheria kujiridhiwa, walio na haki watapewa haki yao.

Hata hivyo, Makalla alisema iwapo wanaodai kuwa wamiliki itabainika ni haki yao, kinachoweza kufanyika ni mazungumzo ya pamoja baina yao na mamlaka husika ili waweze kulipwa fidia eneo hilo likabaki salama mikononi mwa serikali.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini, Laurent Mwigune alisema uwanja huo bado unahitajika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kufungua chuo cha mafunzo ya urubani na ufundi wa ndege.
ILI UPATE HABARI ZETU KWA URAHISI BOFYA HAPA KUINSTAL APPLICATION YA MZALENDO HURU KWENYE SIMU YAKO

About Unknown

About Mzalendo Huru Staff:

Send us your articles, questions, feedback, suggestions, press releases and all others to Whats app on +255657905751
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post