SHEIKH KHAMIS SAIDI MATAKA
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limemteua Sheikh Khamis Saidi Mataka, kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu Taifa ya baraza hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Bakwata, Sheikh Mataka anashika wadhifa huo kutokana na kuwa na elimu ya kutosha ya masuala ya dini pamoja na elimu aliyopata katika vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi.
Taarifa ilisema elimu na ujuzi wa Sheikh Mataka katika fani mbalimbali, vitaisaidia Bakwata kutatua changamoto mbalimbali na kwamba ni mwanzo mzuri wa maendeleo ya Waislamu nchini.
Taarifa ilifafanua kuwa Sheikh Mataka ana shahada ya kwanza ya falsafa ya taaluma za dini na lugha ya Kiswahili aliyoipata katika Chuo Kikuu Huria (OUT).
Aidha, Sheikh Mataka alisomea stashahada ya uzamili katika masuala ya utawala wa rasilimali watu kutoka Chuo Kikuu cha Ignou nchini India kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).