Wananchi wilayani Longido mkoani Arusha wameilalamikia serikali kwa kuwahamisha vituo vya kazi na kuwapandisha vyeo baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo waliotumia fedha zao zaidi milioni mia nne (400) kuchimba kisima eneo wanalojua wazi kuwa halina maji na kusababisha waendelee kuteseka na kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za maendeleo.
Malalamiko ya wananchi hao pia yanatolewa na viongozi wa halmashauri hiyo akiwemo mwenyekiti Bw Sabore Olle Moloiment ambaye amesema watendaji hao pia walikaidi hata maelekezo ya baraza la madiwani jambo linaloonyesha kuwa kulikuwa na ajenda ya siri ya kuhujumu fedha hizo.
Akizungumzia tuhuma hizo mhandisi wa maji wa wilaya ya Longido amesema alikuta sakata hilo linaendelea katika ngazi za juu huku mhandisi wa mkoa wa Arusha Bw.Emanuel Makaidi akidai kuwa hata wao walibaini njama hizo na walishatoa maelekezo lakini pia hayakutekelezwa.
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo ametembelea kisima hicho na kujionea hali halisi na amemwagiza katibu tawala kupeleka taarifa ngazi za juu ili hatua zaidi kwa wahusika zichukuliwe haraka iwezekanavyo.
Wananchi wa vijiji zaidi 30 katika kata 13 za wilaya ya Longido wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji na kwa sasa wanatumia zaidi ya asilimia 90 ya muda wao kufuata maji jambo linaoonyesha wazi kuwa wataendelea kukabiliwa na umaskini.