SIKU chache baada ya gazeti hili kuchapisha ripoti maalumu kuhusu mauaji ya tembo katika Pori la Akiba la Selous na matokeo ya Operesheni Tokomeza Ujangili, mmoja wa waliokuwa washukiwa wa matukio hayo amejitokeza na kueleza maswahibu yaliyomkumba.
Dereva wa zamani wa treni ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), Mahyoro Ismail, ambaye ni mkazi wa jijini Dar es Salaam, amesema vita ya mapambano ya kuokoa tembo ndani ya Pori la Selous, imemsabishia ulemavu wa baadhi ya viungo.
Mbali ya madhara hayo, ameeleza kushindwa kulipa Sh milioni 32 za mkopo wa trekta aliokopa kutoka katika Mfuko wa Pembejeo mwaka 2013 na pia kushindwa kurudishiwa bunduki yake na risasi 15 zilizochukuliwa nyumbani kwake baada ya kukamatwa na kuhusishwa na mauaji ya tembo katika Pori la Selous.
Mahyoro aliyeendesha treni ya Tazara kuanzia mwaka 1977 na kustaafu mwaka 2003, alisema aliamua kukopa trekta kutoka Mfuko wa Pembejeo mwaka 2009 lakini aliweza kupewa trekta hilo na jembe lake mwaka 2013, akiwa na lengo la kulitumia katika kilimo katika eneo la Kisaki, lililo pembezoni mwa pori hilo.
Alisema trekta alilokopa lilikuwa na thamani ya Sh milioni 26.8 na alitakiwa kulipa katika kipindi cha miaka minne na kutakiwa kulipa Sh milioni 32 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, jambo ambalo sasa linamuweka katika mazingira magumu kutokana na kutokuwa na uwezo wa kulipa deni hilo.
Akikumbushia kilichompata Mahyoro alisema kamwe hawezi kuusahau usiku wa Oktoba 28, 2013 saa 7.30 usiku, ambapo alivamiwa na askari akiwa katika mashamba yake katika eneo hilo la Kisaki na kuelezwa kuwa alikuwa anahusika na mauaji ya tembo katika Pori la Selous.
“Nakumbuka ilikuwa saa 7.30 usiku. Nikiwa chumbani ghafla niliona tochi kubwa inanimulika kutokea dirishani. Nilishtuka sana na ghafla nilisikia watu wakijitambulisha kuwa ni askari na kuniamuru nifungue mlango, kwa vile nahusika na mauaji ya tembo,” alisema.
Alisema pamoja na madai hayo kwake, askari hao waliomtuhumu pia kuwa anamiliki silaha mbalimbali zinazotumika kuua tembo ndani ya pori hilo, walimfanyia upekuzi na kushindwa kupata silaha yoyote katika nyumba yake ya shambani Kisaki hadi walipomsafirisha siku kadhaa baadaye kwenda nyumbani kwake jijini Dar es Salaam na kuikuta bunduki aliyokuwa anaimiliki kihalali aina ya Rifle 458 Manlicher yenye namba 18243 na risasi 15.
Pamoja na kueleza madhara mbalimbali yaliyompata baada ya kukamatwa kwake na kushikiliwa kwa siku kadhaa katika Kambi ya Matambwe liliko lango kuu la kuingilia ndani ya Pori la Selous, Mahyoro alisema tukio hilo limemfanya kubaki na ulemavu wa baadhi ya viungo na hasara kubwa.
Sakata la bunduki
Akizungumzia mwito uliotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba alipozungumza na gazeti hili hivi karibuni kwamba walionyang’anywa bunduki katika Operesheni Tokomeza wafike katika vituo vya Polisi wakiwa na leseni zao ili warejeshewe, Mahyoro alisema agizo hilo la Waziri linakabiliwa na vikwazo kadhaa.
“Tunashukuru Waziri (Mwigulu) kupitia gazeti lenu (HabariLeo) ameagiza tufike na leseni zetu kuchukua bunduki zetu, lakini sisi wengine tulinyang’anywa bunduki na leseni yake na kwa muda mrefu sasa mimi binafsi nimekuwa nafuatilia bunduki yangu lakini nimekuwa nazungushwa bila kupata msaada wowote,” alisema.
Mbali ya kuelezea hatua alizozipitia, Mahyoro aliweza kuonesha barua mbalimbali na majibu juu ya kumtaka kuendelea kuvuta subira wakati hatua za kuisaka bunduki yake zikiendelea zikiwemo barua tatu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Barua hizo ni pamoja na ya Agosti 10,2015 iliyosainiwa na Veronica Chacha ambaye ni Wakili wa Serikali Mfawidhi, ya Septemba 8, 2015 iliyosainiwa na Calistus Kapinga na ile ya Februari 24, mwaka huu iliyosainiwa pia na Kapinga, ambazo zote zinamtaka kuendelea kuvuta subira wakati suala la upatikanaji wa bunduki hiyo likifanyiwa kazi.
Barua nyingine ni ile ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya Agosti 4, mwaka huu, iliyosainiwa na Keraryo H.W inayomtaka pia kuendelea kusubiri; hatua ambayo Mahyoro alisema inatia shaka agizo la Waziri Mwigulu kutekelezeka, huku akimuomba Waziri huyo kumsaidia aweze kupata bunduki hiyo.
Sakata la Mkopo
Alisema tukio la kukamatwa kwake pia lilisababisha madhara makubwa kwani aliporejea alibaini trekta alilokuwa amekopa kutoka Mfuko wa Pembejeo kuibiwa vifaa mbalimbali nyumbani kwake Kisaki na kutokana na ukosefu wa fedha za kununua vipuri vilivyoibwa hadi sasa ameshindwa kuendelea na shughuli za kilimo na hivyo kukosa fedha za kurejesha mkopo.