Maandamano baada ya muuza samaki kukanyagwa na lori hadi kufa nchini Morocco |
Maelfu wa raia wa Morocco walifanya maandamano wikendi hii katika miji kadhaa baada ya muuza samaki mmoja kukanyagwa hadi kufa na lori la kubeba takataka alipokuwa akijaribu kuchukua samaki wake ambao alikuwa amepokonywa na maafisa wa polisi.
Kifo cha Maouhcine Fikri katika mji wa kaskazini wa Al-Houciema siku ya Ijumaa kilizua hasira kali miongoni mwa raia katika mitandao ya kijamii.
Kifo chake kinafananishwa na kile cha muuza matunda wa Tunisia mwaka 2010 ambacho kilisababisha maandamano makubwa.
Mfalme wa Morocco King Mohammed VI amewaagiza maafisa wake kutembelea familia ya Fikri.
Wizara ya maswala ya ndani pamoja na ile ya Haki zimeahidi kuanzisha uchunguzi.