Dar
er Salaam. Kijana Abdullatif Hamisi (23), amemwandikia barua Jaji Mkuu
akilalamikia hatua ya Mahakama Kuu kutoa hukumu mbili tofauti na
kumnyima haki ya kupata mgawo wa urithi wa mali ya baba yake.
Hamis
amemweleza Jaji mkuu kuwa yupo hatarini kupoteza haki yake ya urithi
aliyoipigania tangu 2006 baada ya baba yake, Mohamed Hamis kufariki
dunia.
Alisema
nyumba ya baba yake ya ghorofa mbili iliyopo katikati ya Jiji la Dar es
Salaam kwenye kiwanja namba 9 kitalu ‘A’ Mtaa wa Aggrey ikiwa na hati
ya umiliki namba 56967, imeuzwa kwa Sh400 milioni.
Hata
hivyo, Hamisi alidai pamoja na kushinda kesi Mahakama Kuu iliyoamuru
apewe mgawo wake katika mauzo hayo, Mahakama hiyo hiyo kitengo cha Ardhi
imempoka tena haki hiyo.
Kwa
mujibu wa hukumu ya kitengo hicho cha Ardhi iliyotolewa na Jaji
Fredrica Mgaya, Desemba 23, 2015, nyumba hiyo ya urithi sasa ni mali ya
mfanyabiashara, Mehboob Yusuf Osman.
Mkataba
wa mauziano kati ya mmoja wa wasimamizi wa mirathi unaonyesha moja ya
sharti la mauziano hayo ni kwa msimamizi huyo naye kupewa sehemu
(apartment) katika nyumba hiyo. Hata hivyo, Sheria ya Mirathi inakataza
msimamizi wa mirathi kuwa mnufaika wa mali za marehemu.
Nyaraka
za kimahakama ambazo gazeti hili inazo zinaonyesha mkataba wa mauziano
ulifanyika mwaka 2006, lakini haionyeshi kama kuna mahali ambako
msimamizi alishatoa taarifa hizo wakati kesi ikiendelea kortini.
Kutokana
na mgongano huo, Hamis amemwandikia barua Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman
Chande akimuomba afanye mapitio ya dharura kwenye jalada la kesi hiyo
ili kuepusha haki yake kupotea.
