Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Elisha Hilal alisema juzi kuwa Dk Tubutu amehamishiwa Wilaya ya Kibondo, Mkoa wa Kigoma na nafasi yake kuchukuliwa na Dk Amon Mremi kutoka Wilaya ya Longido, Mkoa wa Arusha.
“Sisi tulishamchukulia hatua kwa kumsimamisha kazi na kumtaka ajieleze kwa nini asichukuliwe hatua zaidi za kinidhamu kulingana na sheria, kanuni na taratibu za ajira, lakini mwajiri wake amemhamishia kituo kingine cha kazi,” alisema mwenyekiti huyo.
Sakata la mganga huyo liliibuka wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella wilayani Magu baada ya taarifa ya utendaji kueleza kuwa hajaonekana kazini kwa zaidi ya wiki mbili bila kutoa taarifa yoyote.
Kufuatia taarifa hiyo, Mongela aliliagiza baraza la madiwani la halmashauri hiyo kumchukulia hatua mganga huyo, agizo ambalo lilitekelezwa kwa wakati.
Akizungumzia suala hilo, Mongela alisema ofisi yake haina pingamizi na uhamisho wa mganga huyo kwa sababu umefanywa kwa ridhaa ya mwajiri wake.
“Kama mwajiri wake kamhamisha hatuna neno tunamtakia kila la heri huko aendako,” alisema Mongella
Hata hivyo, mmoja wa wakazi wa Magu, Miriam Mussa alisema kitendo cha daktari huyo kuhamishwa kabla ya uchunguzi na hatua dhidi yake kuchukuliwa kutokana na tuhuma zilizokuwa zikimkabili ni mwendelezo wa mazoea ya kuhamisha matatizo kutoka kituo kimoja cha kazi kwenda kingine.
“Huyu alisimamishwa kwa kutofika kazini bila taarifa, sasa anahamishiwaje kituo kipya cha kazi kabla ya masuala hayo kuchunguzwa na kumalizika?” alihoji Miriam.
Juhudi za kumpata mganga huyo kuzungumzia tuhuma za utoro zilizokuwa zikimkabili na uhamisho wake hazikuzaa matunda baada ya aliyepokea simu yake kudai ilikuwa eneo la kuchajia na kuahidi kumpa taarifa akirejea na baadaye simu hiyo iliita bila kupokelewa.
